Tuesday, September 4, 2007

Tanzania kutoka utandawazi mpaka hari mpya

Naamka asubuhi nafungulia redio nakutana na taarifa inayazungumzia kuwa serikali imeamua kuanzisha shule za secondary katika kila kata,nilifurahi sana kwani ni kama ndoto,nikasema sasa taifa litakua limejikwamua katika swala la elimu,na watoto wa walala hoi wataweza kutoboa mpaka vyuoni sasa.lakini gafla kengele ya hatari ikaita kichwani mwangu,nikajiuliza hivi mpango huu wa kuanzisha shule katika kila kata sio kama utakua umeharakishwa sana? Maana ki msingi Taifa lipo katika hali tata kuhusu waalimu,iweje leo serikali itake kuwa na shule za kata?

Ni busara kama serikali ingeamua kuweka swala hili kama mpango mkakati wa muda mrefu na sio kukurupuka,kwa mtazamo wangu mimi niliona kuwa serikali ingeanza na mpango wa kupeleka waalimu shule kwa muda wa miaka mitano,hapa namaanisha wangeweza kuwa na waalimu waliofuzu wakutosha alafu swala la kujenga shule lifuate.

Kutokana na kukurupuka serikali inapeleka wanafunzi wa form six kwenye mafunzo ya uwalimu kwa mwezi mmoja,matokeo yake tunakuwa na waalimu ambao

hawajajifunza vizuri hasa mbinu za ufundishaji na jinsi ya kuishi na
wanafunzi,unajua nini kinafuata hapo,ni kuwa na wahitimu ambao hawataweza kutuwakilisha kimataifa,pia tutapata madaktari feki,wahasibu wakughushi,na wataalamu wa kusuasua.

Kabla sijatoka kitandani nasikia matokeo ya kidato cha sita yametoka,nikapata mshituko kwani nina ndugu zangu waliohitimu mwaka huu,kabla sijakaa sawa wanatangaza mwaka huu wanafunzi wamefaulu kwa kiwango kidogo ukifananisha na mwaka jana,nikafikiria sasa ule mpango wa serikali kuanzisha shule za kata utasaidia kufaulisha wanafunzi au ndio utadidimiza? Jibu tunalo wenyewe!

Wakati naendelea kujiuliza nikapata kitu kingine,kuwa waalimu wenyewe wanaokwenda kwenye hiyo crash program ni kati ya wanafunzi walioshindwa kidato cha sita,swali je kama mtu anaekwenda kusomea uwalimu alifeli atawezaje kumfundisha mtu akafaulu? Siku hizi utaalamu wa uwalimu uchukuliwa na watu ambao wameshindwa kujiunga sehemu zingine,wanafanya uwalimu ni sehemu ya kukimbilia,kwa mtindo huu tutafika? Serikali itaweza kufikia malengo ya MKUKUTA? Jibu sijui….

Naendelea kutafakari hali halisi ya uchumi kwa jamii nzima nashindwa kupata jibu,hali ni mbaya kwa taifa nzima,watu hawana pesa,ajira zimekuwa dhahabu,kuna wakati nikajiuliza hivi hali hii ya uchumi itadumu mpaka lini? Au ndio hari na kasi mpya? Maana mfumuko wa bei ndio huwooooo!!!! Kodi za bidhaa ndio hatuelewi hatima yake kwani kila kukicha vitu havishikiki,lakini kwasababu hii ni nchi ya kitu kidogo watu wanamezea na siku zinakwenda.

Kelele za viongozi hivi sasa ni kuhusu kujiajiri (ujasiriamali),viongozi hao ambao wanapiga kelele za ujasiliamali hawajawahi kuwa hata na kibanda cha kuuza nyanya,ni wepesi sana kuimba ujasiliamali lakini kuutekeleza nikasheshe,ujasiliamali hausimami wenyewe kama baadhi ya vitu kama sera nzuri za nchi,kodi zinazovutia kwa biashara zinazoanza,Elimu itolewe juu ya ujasiliamali,kuzuia vitu kutoka nje visilete ushindani na uwepo wa taasisi za fedha ili kuwezesha wajasiliamali,vitu hivi vikiwepo basi tunaweza zungumzia ujasiliamali.

Kuna mtu mmoja aliniambia aisee serikali ya sasa mikopo njenje,nikamuuliza mikopo ipi hiyo? Akasema si ya kikwete? Ni kamuuliza umeshachukua hapo? Akasema ipoo! Ipo umepata? Hapana,hiyo ndio nchi ya watu wadogo.

Mzee zamani kulikua na kodi ya kichwa watu walikuwa wanaacha familia zao na kukimbilia porini,ilikuwa inatenganisha familia haswa,kipindi hicho watu walikuwa sio wavumilivu na sehemu za kukimbilia zilikuwepo,sasahivi kodi zilizopo hazina tofauti na hiyo kwani mtu anapokea mshahara ambao ukiuangalia kodi ni kiasi kikubwa mpaka unakata tamaa,kama haitoshi basi mtu huyohuyo anatozwa kodi katika bidhaa atakazonunua,sio hiyo tu nauli za daladala nazo zipo kwenye chati,kwa mishahara yetu ya koma moja ndani ya wiki mbili hauna pesa unageuka kuwa ombaomba,sasa unajiuliza hivi nafanya kazi au nafanyia watu kazi? Je mtu huyu akiamua kukimbilia nje ya nchi atakuwa ametofautiana na aliyekuwa anakimbia kodi ya kichwa? Jibu tunalo.

Maisha ya watanzania wengi ni ya kusuasua,ndio maana unakuta mtu anamiaka juu ya thelethini bado hajaoa,sio kama hapendi kuoa bali mambo hayajakaa sawa,swali ni lini mambo hayo yatakaa sawa? Watu haohao wanakufa sababu ya umri na kuziacha familia zao changa zinateseka.tulio wengi mamboyanaanza kuwa ya afadhali tukiwa na umri wa kuitwa babu,mtu huyohuyo unakuta hajatoka kwa baba na mama wakati nchi zilizoendelea mtoto anapokwenda chuo kikuu akirudi uko anaanza kujitegemea mwenyewe wala hatopokelewa nyumbani.,hapo ndio utajua unaishi katika nchi hipi? Kwanini tusikimbilie marekani kutafuta maisha? Unafikiri waliokwenda uko wakina ndesanjo,egidio,liganga,john selemani na ibra watarudi tena wakikumbuka jua kali la bongo?.....ngoja tuwasubiri.au uanasemaje mzee chemsha bongo?

Nikiwa mdogo baba yangu aliniambia uku akiwa amekaza meno na macho kuwa nisioneshe hisia zangu wakati wote,iwe nina tatizo au raha,mara ya kwanza nilishindwa kumuelewa alikua anamaanisha nini lakini nilikuja kumwelewa baada ya kujua kuwa mara nyingi tamaduni zetu zinawafanya wanaume kuwa wastahimilivu,na wala sikumbuki ni lini baba aliwahi kunikumbatia na kunipongeza kwa jambo zuri nililowahi kutenda,sasa unaweza kuona ni jinsi gani hata mzazi anamlea mototo wake katika hali ya shida kwani yeye mwenyewe anatambua kabisa kuwa lazima tutapata tabu uko mbeleni,lakini hii sio kawaida kwa nchi za wenzetu.

Itafikia wakati tutahita kumjua mchawi wa nchi yetu ni nani? Na pindi tukimjua lazima tutamfanyia kazi ipasavyo,kwani mtu huyu ni mbaya sana katika maendeleo ya nchi hii yetu ya kitu kidogo.

Tunatambua kuwa uwongozi ni kazi nzito sana tena ni ya kubeba dhamana ya walalahoi walio wengi,hivi unafikiri mtoto mdogo ukiwa unamchapa kila siku bila sababu mwisho wake unafikiri ataendelea kuvumilia tuu? Ipo siku atachoka na kuamua kukurudishia,vivyo hivyo hata watanzania watachoka na kuamua kuchukua maamuzi yatakayo shangaza dunia,siombei iwe hivyo lakini huo ndio ukweli mzee.

tuonane wakati mwingine mzee mkubwa.

5 comments:

Egidio Ndabagoye said...

Karibu sana Honest katika ulimwengu wa blogu.Kiti chako kilikuwa wazi muda mrefu sasa unakaribiswa saana kaa kitini utupashe meengi

Uchambuzi murua kaka.

Simon Kitururu said...

Karibu Mkuu!Kazi nzuri!

Honest Peter said...

Asante sana tupo pamoja

chemshabongo said...

yap! hii sasa safi ile yakwanza nilikuwa naumia macho kuicheki si unajua blac and white tena? sasa naamini kazi imeanza rasmi. tupo pamoja

mwandani said...

Karibu sana.